MAMA LORAA AMSAIDIA MTOTO ALIYEKUWA AKIBAKWA NA BABA YAKE MZAZI
Na Christopher Lissa
Mdau maarufu wa sanaa ambaye pia ni mwenyekiti wa kundu la kina mama lililojikita kusaidia wanawake na wasichana walio katika maisha magumu la Hybiscus Women Group, Catheline Ambakisye 'Mama Loraa', ametoa msaada wa pesa taslimu Sh.200,000 kwaajili ya kuisaidia familia ya Bw. Athanas Ngomani mkazi wa Mbondole, Ilala ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kumbaka na kumnajisi binti yake wa kumzaa(jina linahifadhiwa).
Akikabidhi msaada huo kwa mama wa binti huyo Bi. Tumaini Kabeja, ambaye ni mke wa Bw. Athanas, Mama Loraa amesema kuwa ameguswa mno na tatizo la mtoto huyo ambalo linadhihirisha ukatili mkubwa kwa watoto wa kike suala ambalo amesema ni miongoni mwa majukumu ya kundi la Hybiscus Women Group ambayo wameamua kuyavalia njunga.
"Huu ni ukatili kwa wanawake. Baba kulala na binti yake tena binti mdogo ni kitendo cha kikatili mno. Nataka ufike wakati kwa jamii kupaza sauti kupambana na unyama huu.Watoto pia wanaofanyiwa ukatili wa aina hii waamke. Wasiogope vitisho, watoe taarifa polisi au kupitia vyombo vya habari ili wahusika washughulikiwe.Sheria zipo zitachukua mkondo wake"alisema Mama Loraa.
Alimshauri Bi. Kabeja kutumia pesa hiyo kwa shughuli za ujasiliamali kwa kuendesha biashara ndogo ndogo kwaajili ya kujikwamua kiuchumi.
Alisema kuwa, Hybiscus Women Group baada ya kuona tatizo la unyanyasaji wa jinsia linazidi kuota mizizi katika jamii wameamua kuandaa filamu iitwayo Machozi ya Mtoto wa Kike 'Girl's Tear' ambayo itazinduliwa May mwaka huu ambayo itatunisha mfuko wa kupambana na matatizo ya wanawake walio katika mazingira magumu.
"Filamu hii itakuwa ni sauti kwa watoto wa kike wanaoteseka. Ni filamu ya kusisimua mno na yenye kisa cha kweli. Imeshirikisha wasanii wengi wakubwa, kama kina Bi. Mwenda, Anitha wa Kidedea, Ben, Sandra , Mwanamtama, Ana Ndunguru na mimi mwenyewe"alisema.
Akipokea pesa hizo, Bi. Tumaini alimshukuru Mama Loraa kwa msaada huo ambao amesema kuwa ni muhimu kwa sasa.
"Kwa kweli nimefarijika mno, namshukuru sana Mama Loraa kwa msaada wake.Pesa hizi zitatusaidia sana kufanya biashara na shughuli za ujasilia mali. Kwa kweli hali ya maisha ni ngumu sana" alisema Bi. Tumaini.
Katika toleo lake lililopita gazeti hili liliandika kuhusu habari ya Bw. Athanasi kulala kimapenzi na mtoto wake mwenye umri wa miaka 16 kuanzia binti huyo akiwa darasa la tatu ambapo hivi sasa binti huyo anasoma darasa la saba. Athanas anadaiwa kumuingilia binti huyo kinyume na maumbile pia ambapo binti huyo aliamua kutoboa siri hiyo baada ya kushindwa kuvumilia ukatili wa baba yake.
No comments:
Post a Comment