Wednesday, June 6, 2012

HILI NI BONGE LA HADITH WADAU YAANI HUTAKIWI KULIKOSA

MZIMU WA MAUTI
(The Ghost of Death)
Mtunzi :Christopher Lissa -1

Ni unyama, mauaji, ukatili na visasi vya kufa mtu.Damu nzito inamwagika.Nini chanzo na hatima yake? Anza kujiramba


Iilikuwa ni asubuhi njema! Yenye kila dalili za baraka zote ndani yake.

Wingu lenye rangi nzuri ya blu bahari ilitamarahaki mbinguni na kumfanya kila aliyetazama juu kuelewa fika kuwa kulikuwa hakuna dalili yoyote ya mvua siku hiyo

Kiupepo murua cha bahari ya Hindi kilikuwa kikivuma kwa madaha kutoka katika baharini na kuleta burudanaani tele jijini Dar es Salaam.

Baada ya kufanya mazoezi, nilijimwagia maji na kuuramba, tayari kwa kuelekea kwenye mihangaiko yangu ya kila siku.



Nilikuwa siwezi kutoka ndani bila kumbusu mke wangu Ladhia na mtoto wangu kipenzi Janeth aliyekuwa na umri wa miaka sita.

Kwa ujumla niliwapenda mno.Kwa jinsi nilivyokuwa nawapenda sikuelewa ninani ninayempenda zaidi.Mama au mwana!Nilitamani muda wote niwe ninawaangalia tu. Nikicheza nao kwa furaha.

Kwakweli tuliiishi kwa raha mstarehe.Nyumba ilitawaliwa na upendo tele.Nilimkubatia mke wangu Ladhia nikambusu na nikamalizia na mwanangu Janeth.

Hapo nikachuchumaa kidogo na kumkumbatia pia.

"Jane..mchumu dadii" nilisema.
"Mmmwaaa!mmwaaa..mmwaaaaa” mwanangu Janeth Akanichumu shavu la kulia kisha la kushoto na kumalizia busu lake katikati ya paji langu la uso.

Hakika nilijisikia raha ikibubujika ndani ya moyo wangu.Nami nikammwagia mabusu mazitomazito uso wote.

Ilikuwa ni kasumba yangu kufanya hivyo kila nilipokuwa nikitoka nyumbani.

"Unataka nikuletee nini mwanangu?" nikamuuliza.
"Dadii mi nataka Chocolate na bisi" alisema mwanangu Janeth.
"Haya nakuletea mwanangu mzuri " Nikamnynanyua na kumbemba kwa kumkumbatia kifuani.
"Na wewe mke wangu nikuletee nini?"
"Epple na Soseji tu mume wangu"
"Sawa mpenzi.Mmbaki salama" nilisema baada, huku nikimpa mke wangu motto ambembe.MKe wangu akampokea.
Mara simu yangu ya mkononi iliita kwa fujo.Nikaitoa mfukoni na kutazama.Nilibaini kuwa ilikuwa namba ngeni.Nikaitazama tena namba hiyo sikueielewa.
Nikaamua kuipokea hivyo hivyo huku nikiitegesha vizuri simu katika sikio langu la upande wa kushoto.
"Ndiyo, niambie" nilianza kuongea.
"Hapo naongea na mwandishi wa habari wa gazeti la Sani?" sauti ya kiume kutoka kwenye simu ilipenya katika masikio yangu barabara.
"Ndiyo mimi.Naitwa Chriss.Nani mwenzangu?"
"Ndgu yangu , mimi ninaishu hapa, tunaweza kuonana haraka?"
"Ishu gani hiyo na uko wapi?"
"Niko Dar Kurasini hapa.Kama unaweza njoo haraka, nina picha na kila kitu"
"Lakini niambie kwa ufupi habari inahusu nini kaka"
"Njoo! Chriss.Fanya haraka"
"Ok! Nakuja, nisubiri"

Nilikata simu.Nikatafakari kidogo juu ya wito huo wa ghafla.Mara nyingi nilikuwa makini sana katika kazi yangu hii ya uandishi wa habari.

Nilijua fika kuwa nilikuwa nimezungukwa na maadui wengi ambao tulitofautiana katika kazi yangu hii.

Mara nyingi niliwahi kupigiwa simu nyingi za mitego ya maadui wangu.Nilinusurika mara kadhaa kuuawa au kufanyiwa unyama.

Mafunzo ya kikachero niliyokuwa nimepata chuo cha Polisi CCP Moshi yaliniwezesha kumudu sana kukabiliana na changamoto katika kazi hii.

Hakuna aliyejua kuwa nilikuwa shushu wa Polisi na kachero hatari.Hata mke wangu Ladhia alikuwa hajui siri hii.

Waandishi wengi na wadau walinichukulia kama paparazi wa kawaida tu na hata hao maadui zangu ambao hawakunijua kiundani waliniona mwandishi wa kawaida.

*************
Mwendo wa kutoka nyumbani kwangu Mtoni Kijichi Temeke, nilipokuwa naishi hadi kurasini haukuwa mrefu.

Niliona ni vema nikatumia pikipiki yangu kubwa aina ya Kawasaki ili niweze kuwahi kufika,kwa sababu ya kukwepa foleni ya magari barabarani.Nilichukua begi langu lenye vifaa vyote vya uandishi wa habari vikiwemo, kamera na tape recorder.

Nikajitoma kwenye Pikipiki na kuanza safari ya kuelekea Kurasini.
Nikiwa makutano ya barabara za Kilwa na Kawawa eneo la Uhasibu mara simu yangu ikaita.

Nilitoa simu na kutazama.Niliona ni ile namba ya yule mtu aliyedai ana habari kule Kurasini.Nikapokea, huku nikitumia mkono mmoja kuendesha pikipiki.

Nilishika barabara ya Shimo la udongo!Huku nikiwa naongea na simu kwa umakini.

"Niko mataa hapa Uhasibu ndiyo na kuja huko wewe uko wapi?" nilimuuliza.
"Njoo mpaka karibu na Baraza la Maaskofu hapa.Utaniona barabarani nimevaa kanzu na kiremba kichwani natembea kando ya barabara" ilisema sauti ya mtu huyo.

Kwa kuwa nilikuwa nikiendesha Pikipiki kwa kasi ile nakata simu tu nilianza kumuona mtu huyo mbele yangu. Nikaanza kupunguza mwendo ili nimsome kwanza.Asije akawa mtu hatari kwangu.

Nikasimamisha Pikipiki na kuchukua simu.Nikampigia.Nikaona akisimama na kuweka simu yake sikioni huku akiangazaangaza macho huku na kule.

"Uko wapi?" nikauliza
"We uko wapi shekhe, mi niko bado Kurasini hapa?"
"OK! Nimekuona!Nakuja" Nikakata simu na nikaona yule mtu akiwa amesima akiangaza macho huku na huku kunitafuta.Nilijua hanijui.Nikawa sina wasiwasi naye.

Wakati nawasha Pikipiki ili nimfuate, niliona gari moja aina ya BMW Saloon rangi ya blu ikiingia upande aliokuwepo yule mtu.Ilikuwa ikienda mwendo wa kasi.

Ilipomkaribia ikapunguzamwendo.Mara vioo vya gari hiyo vilishushwa upande aliokuwepo.Mitutu miwili ya bunduki ikachomoza dirishani.

Ghafla milio ya risasi ikaanza kulindima, zilikuwa zikimiminika kama mvua.

Risasi zilimchakaza mwili mzima yule mtu hadi alipodondoka chini, na kulala chali.

Tayari kamera yangu ilikuwa mkononi ikichukua tukio zima.Gari hiyo iliondoka kasi na kutokomea.

Watu walitawanyika huku na kule wakikimbia.Kwa kuwa mimi nilikuwa na moyo wa kikachero, nilikwenda kwa haraka pale ulipokuwa umelala mwili wa yule mtu.Nikaupekekua kwa haraka mwili wake.

Ndani ya Kanzu nilikuta bahasha ndogo na kitu kama Tape Recoder, ya kisasa yenye uso wenye kama kamera ya video.Nikavichukua.Hata hivyo simu yake sikuiona.Niliangaza huko na huko bado sikuiona.

Mara nikasikia ving'ora vya gari za Polisi kwa mbaali.Sikutaka kupoteza muda.Nikapanda kwenye pikipiki tayari kwa kutoweka enehilo.

Wakati naondoa pikipiki niliona watu wawili waliokuwa wamepakizana kwenye Pikipiki wakirekodi kwa video kamera.

Nilishituka kidogo, hata hivyo sikutaka kupoteza muda hapo.Mawazo yangu yalikuwa ni kwenye ile Tape Recorder na ile bahasha ya kaki.Kulikuwa nanini.

Nilichukua vitu hivyo kwa sababu jamaa alinieleza kwenye simu kuwa alikuwa na habari.Niliamini kuwa habari lazima itakuwa ndani ya bahasha au kwenye Tape Recoder hiyo.Nilitaka kuijua ni habari gaini na kwanini auawe kabla hatujaongea?Kwanini?Kunanini nyuma ya mapazia juu ya habari hiyo?

Nilipishana na gari mbili za Polisi aina ya Pick Up Landcruiser zilizokuwa na Polisi wachache ambao wengi walivaa kiraia wakiwa na bunduki.

Hata hivyo wazo lilinijia kuwa, ningepata picha nzuri zaidi wakati Polisi wakiuchukua mwili wa yule jamaa.

"Nirudi eneo la tukio!?Je hakuna raia walioniona wakati naupekua ule mwili? Si watanishuku kuwa nashirikiana na na wauaji.Mh!"nilijisemea huku nikipunguza mwendo wa Pikipiki na kuingia katika mzunguko wa barabara ya Kilwa na kuanza safari ya kurejea nyumbani.

********

Nilipofika nyumbani nikaingiza Pikipiki getini na kufunga geti.Nikaingia ndani na moja kwa moja na kuelekea chumbani.Hata hivyo nilihisi kama kengere ikigonga kichwani mwangu kuwa nyumba ilikuwa kimya sana.

Sikumuona mke wangu wala mtoto.Kibaya zaidi niliona milango yote iko wazi.

"Mama Janeti!" niliita, hata hivyo hakuitikia.
Nikafunga mlango wa nje kwa umakini kisha nikaendelea kumuita mke wangu.Nilijua pengine atakuwa chumbani.Huko nako sikumuona.

Nikaamua kumpigia simu, nilishangaa kuwa ilikuwa haipatikani.Nilighutuka sana nilipoona pete ya ndoa ya mke wangu ikiwa kitandani.

Kitanda kilikuwa kimevurugika.Haikuwa kawaida.

Nikaichukua pete ya ndoa ya mke wangu na kuitazama kwa makini.Nikajua lazima atakuwa bafuni, kwani alikuwa na tabia ya kuvua pete kila anapoingia bafuni kuoga.

Hata hivyo nikajiuliza, kwanini asiogee bafu la chumbani, badala yake akaogea bafu la wageni?

Niliamua kwenda huko kwenye bafu la wageni.Nilisikia maji yakimwagika.Sikuwa na hofu kuwa ni kweli mke wangu alikuwa anaoga.Lakini je alikuwa anaoga pamoja na mtoto?

Nikagonga mlango wa bafuni na kusikilizia.

"Mama Janet..mama Janet.." niliita, lakini mlango haukufunguliwa na maji yaliendelea kumwagika.Nikajaribu kufungua.Ukafunguka.
Itaendelea

Pia unaweza kuisoma hadithi hii kila siku litokapoa gazeti lako pendwa la SANI. Jumasi na Jumatano.

No comments:

Post a Comment